WANAJESHI wastaafu nchini wamevitaka vyama vinavyounda umoja wa Ukawa kufuta usemi wake kwamba wapo wanajeshi wastaafu waliojiunga nao kwa ajili ya kusaidia mikakati ya kufanikisha ushindi wao. Walitoa kauli hiyo kwenye kikao cha pamoja baina ya wanajeshi hao wastaafu na viongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) uliokuwa ukilenga kutoa elimu na hamasa kwa wanajeshi hao wastaafu kujiunga na huduma za matibabu za mfuko huo. Wakizungumza katika kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa NSSF mjini Kigoma, wanajeshi hao wastaafu wamesema kuwa kauli ya Ukawa imewadhalilisha na wametaka kuombwa radhi kwa hilo. Mwenyekiti wa Muungano wa Wanajeshi wastaafu nchini (Muwawata), Assedy Mayugi alisema madai kwamba wapo wanajeshi wastaafu 200 kila mkoa waliojiunga na umoja huo ni upotoshaji kwa umma. Akisoma tamko kwa niaba ya wanajeshi wastaafu wa mkoa Kigoma, Kibwana Shomari alisema wanajeshi wastaafu wa mkoa Kigoma bado watiifu kwa Amiri Jeshi mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali iliyopo madarakani. “Kiapo tulichokula cha kuwa watiifu kwa amri jeshi mkuu wa majeshi ya ulinzi ya wananchi wa Tanzania na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tunaendelea kuwa watiifu kwa serikali iliyopo madarakani,” alisema. Akizungumzia huduma za matibabu zinazotolewa na mfuko huo, Meneja wa NSSF mkoa Kigoma, Josephat Komba alisema wanajeshi hao wanayo fursa nzuri ya kujiunga na huduma hiyo na kupata matibabu katika kiwango knachostahili. Komba alisema wanajeshi hao wastaafu wakijiunga na huduma za matibabu za mfuko kwa kuchangia kila mwezi, watapata matibabu na wategemezi wao.
Wednesday, October 14, 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment